Romans 12

Maisha Mapya Katika Al-Masihi

1 aKwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 bMsifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

3 cKwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. 4 dKama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 evivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Al-Masihi, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 fTuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 gKama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 hkama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

Alama Za Mkristo Wa Kweli

9 iUpendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 jPendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 kMsiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. 12 lKuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. 13 mChangieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

14Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani. 15Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao. 16Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

17 nMsimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. 18 oKama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. 19 pWapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. 20 qBadala yake: “Kama adui yako ana njaa, mlishe;
kama ana kiu, mpe kinywaji.
Kwa kufanya hivyo,
unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

21Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.
Copyright information for SwhKC